Msanii wa Hip Hop, Fid Q amejikuta kwenye wakati mguu mara baada ya kuanza kushambuliwa na Mameneja wa WCB, Babu Tale na Mkubwa Fella mtandao. Hii ni kutokana na Fid Q kufanya tangazo la Fiesta ambalo wamelitafsiri ni kama kijembe kwao (Wasafi Festival).
Mameneja hao wamekuwa wakimshambulia Fid Q kwa madai kuwa licha ya kufanya muziki ameshindwa hata kununua gari dogo tu.
Sasa Fid Q amejibu hilo kwa urefu zaidi kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kueleza kuwa haoni kama ni busara kwa yeye kuchaguliwa watu wa kufanya naye kazi.
==>> Hiki ni kile alichoandika;
Keki ya taifa ni kubwa sana na ina vipande vingi vya kuwatosha wachakarikaji wote wenye kuistahiki. Na kwakua Allah ndio mtoaji riziki, mimi kama mimi sina hayo mamlaka au hata hiyo roho mbaya ya kutamani wachakarikaji wenzangu mkwame katika harakati zenu.
Ninasema hivi ni kwasababu siku zote huwa siamini kama nitapungukiwa kitu nyinyi mkifanikiwa na siamini hivyo kwa sababu ninajiamini mimi ni mchakarikaji na kipande changu cha KEKI bado kipo mezani kinaningojea (cha muhimu ni PUMZI na DUA tu ).
Ni ukweli tupo kwenye tasnia moja na kila mmoja wetu anajaribu kufanya lile alionalo sahihi ili kusogea mbele, na iko wazi mmeshafanya na mnaendelea kufanya mengi makubwa, nami bila kusita siku zote nimekua ni mtu wa kuwapongeza iwe kwa njia ya mitandao au tukutanapo ana kwa ana, mie hufanya vile kiroho safi pasina chembe yoyote ya unafiki.
Nimeyasema hayo hapo juu ili tu uweze au muweze kupata picha halisi ya kilichomo moyoni mwangu na pia kuwakumbusha ya kwamba mimi pia ninao uhuru wa kufanya shughuli zangu za sanaa na yeyote ambaye nimeridhia nae kimaslahi pasina kujali kama jicho la pembeni yangu linaiona faida iliyopo au laah.
Sioni ni busara kwa nyie kuja na kujaribu kunipangia yupi nifanye nae au yupi nisifanye nae ili kuwaridhisha machoni/ mioyoni mwenu.. na kama mnaamini ni haki yenu ya msingi mimi kuyafuata hayo matakwa yenu basi naomba nikujuzeni ndugu zangu mtakua mmeonyesha UBINAFSI wa hali ya juu kwenye hili.
Pia kumbukeni mimi pia nishawahi kuwa na matatizo na MJENGO.. lakini nilijikuta ninapambana peke yangu hadi UTULIVU uliporejea pasina msaada wa mtu yeyote na sikupambana peke yangu kwasababu hamkua na taarifa, taarifa mlikua nazo lakini ninafikiri mlikua mmetingwa na shughuli zenu za ujenzi wa taifa kiasi kwamba hamkuona kama kuniongezea nguvu ingesaidia lile zoezi kuisha haraka.
Kiukweli yale maneno ya kwenye promo ya“MOJAKUBWA”sikutegemea kama yangekua na uzito huu uliopelekea ndugu yangu uchafukwe kiasi cha kunifungulia bomba la matusi humu Insta..
kwanza sikumbuki hata kama niliyatamka kwa nia ya kuleta msigishano huu lakini kama kweli nimewakwaza... Naomba mnisamehe kibinadamu kwa hilo, naomba tumuache SHETANI apite na mwisho naomba nimalize kwa kusema BURUDANI sio VITA.
Fid Q Avurugana na Mameneja wa Diamond Kisa Tamasha la Wasafi Festival
Reviewed by mjtheaction
on
November 21, 2018
Rating:
No comments: